IQNA

Je, iwapo aliyetekeleza hujuma ya kigaidi Las Vegas angelikuwa ni Muislamu?

11:55 - October 08, 2017
Habari ID: 3471208
TEHRAN (IQNA)-Hujuma ya kigaidi hivi karibuni katika mji wa Las Vegas nchini Marekani imetajwa kuwa ufyatuaji risasi mbaya zaidi hadharini nchini na pia tukio hilo limeashiria kuwepo hisia mseto dhidi ya Waislamu.

Kujiri vitendo mbali mbali vya kigaidi duniani kumeandamana na kuenea chuki dhidi ya Waislamu na Uislamu kutokana na watu wanaotekeleza hujuma hizo kuonekana kuwa na majina ya Kiarabu au Kiislamu au ni wenye kudai kuwa ni Waislamu.

Kilichowazi ni kuwa iwapo, Stephen Paddock, gaidi aliyetekeleza hujuma ya Las Vegas Oktoba mosi na kuua watu 58 kabla ya kujiua angelikuwa ni Muislamu basi tungelishuhudia misimamo na matamshi tafauti kabisa na ya hivi sasa ya wanasiasa, wananchi wasiokuwa Waislamu na vyombo vya habari.

Ni wazi kuwa kumeshuhduiwa mapendeleo makubwa na ukemaji duni baada ya Paddock kutekeleza mauaji ya umati mkubwa wa watu wakati ambao iwapo mtu anayefungamanishwa na Waislamu angekuwa amemuua hata mtu moja katika umati huo basi kungekuwa na wimbi jipya la hujuma dhidi ya Uislamu na Waislamu. Rais Donald Trump angekuwa anatuma jumbe kupitia akaunti yake ya Twitter kila wakati na kusema, "Niliwaambia” kama anayosema kila mara kunapojiri tukio la ugaidi Ulaya. Bunge la Marekani, Kongres, lingeitisha vikao vya dharura kujadili sheria mpya kuzuia tukio kama hilo kujiri na kuwabana zaidi Waislamu nchini humo. Aidha Waislamu wangeshambuliwa na misikiti kuhujumiwa kote Marekani.

Lakini baada ya kubainika kuwa gaidi aliyeuawa watu 58 wasio na hatia alikuwa Stephen Paddock asiye na ufungamano wowote na Uislamu au Waislamu, na kwamba ni Mmarekani mzungu, sasa inadaiwa kuwa alikuwa na matatizo ya kiakili na kwamba aliweza kumiliki silaha alizokuwa nazo kwa sababu sheria inaruhusu. Baada ya hapo, Rais Trump wa chama cha Republican kinachounga mkono haki ya Wamarekani kumiliki silaha nafanya kila awezalo kuhakikisha kuwa sheria za umiliki silaha hazifanyiwi mabadiliko. Warepublican wanasema ukatili wa Las Vegas haukuhusiana na ISIS au makundi mengine ya kigaidi na hivyo ,haupaswi ‘kutumiwa kisiasa’ hivyo wanataka sheria za umiliki silaha zibakie hivyo.

Hakuna shaka Stephen ni jina la Kikristo, lakini hatujaona ugaidi aliotenda ukifungamanishwa na Ukristo au Wakristo. Huu ni undumakuwili wa hali ya juu.

Pamoja na kuwa Marekani inatuma majeshi yake katika nchi za Kiislamu kwa madai eti ya kupambana na ugaidi na kuwazuia magaidi kuwadhuru Wamarekani, ushahidi umebaini kuwa aghalabu ya vitendo vya kigaidi vya ufatuaji risasi kiholela na kuwaua watu watu wasio na hatua nchini Marekani hutekelezwa na Wamarekani Wakristo au wanaodai kuwa ni Wakristo. Ukweli ni kuwa maadui wakubwa wa Wamarekani ni Wamarekani wenyewe kwani takwimu zinaonyesha kuwa kila mwaka Wamarekani 100,000 hupigwa risasi kila mwaka na kuigharimu nchi hilo dola bilioni 45. Kwa wastani Wamarekani 33,000 huuawa katika vitendo vya ufatulianaji risasi. Hakuna shaka kuwa ugaidi wa Stephen Paddock huko Las Vegas umebaini wazi undumakuwili wa watawala wa Marekani na namna chuki dhidi ya Waislamu na Uislamu ilivyokita mizizi katika mfumo wote wa utawala na umma katika nchi hiyo na nchi zingine za Magharibi.

3464104

captcha