IQNA

Sayyid Hassan Nasrallah

Njama za Marekani, Uingereza za kusambaratisha Hizbullah zimefeli

11:18 - March 09, 2019
Habari ID: 3471868
TEHRAN (IQNA)-Kiongozi wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon Sayyid Hassan Nasrallah amesema kuwa, Marekani ilikuwa na njama kubwa tofauti kwa ajili ya kusambaratisha harakati hiyo mwaka 2006, lakini uimara wake umeweza kusambaratisha njama zote hizo.

Sayyid Nasrallah aliyasema hayo Ijumaa mjini Beirtu katika hotuba aliyoitoa kwa njia ya moja kwa moja kupitia televisheni kwa munasaba wa kumbukumbu ya mwaka wa 31 wa kuasisiwa kamati ya uungaji mkono kwa harakati ya mapambano ya Kiislamu (muqawama) ambapo sambamba na kuashiria suala la vikwazo vya Uingereza na hatua ya London ya kuiweka Harakati ya Hizbullah katika orodha ya makundi ya kigaidi amesema kuwa, tangu mwaka 2011 kulianza njama chafu kwa ajili ya kutoa pigo kwa muqawama. Ameongeza kwamba kuwarejesha nchini Iraq wanachama wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) na pia kuendeleza mashinikizo dhidi ya Lebanon, Palestina na Yemen, ni miongoni mwa njama hizo. Sayyid Hassan Nasrallah amebainisha kwamba hatua ya kuuwekea vikwazo muqawama haitokani na udhaifu wa harakati hiyo, bali inatokana na uwezo mkubwa wa muqawama na kuongeza kwamba, hatua zote hizo chafu ziliratibiwa na Marekani na utawala haramu wa Kizayuni pamoja na nchi za eneo la magharibi mwa Asia.

Akibainisha kwamba huenda pia vikwazo vya Marekani vikashadidishwa dhidi ya mrengo wa muqawama, amesema kwamba, hii ni kwa sababu muqawama umeweza kusambaratisha ajenda chafu za Washington na utawala wa Kizayuni na ambazo zimekuwa zikiungwa mkono na pande kadhaa katika eneo.

Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amebainisha kwamba muqawama ulisimama imara katika kukabiliana na njama za Rais Donald Trump wa Marekani kwa ajili ya kufanikisha ajenda yake kupitia mradi wa 'Muamala wa Karne' ambao unalenga kukandamiza haki za taifa la Palestina na kuupa nguvu utawala bandia wa Israel.

Sayyid Nasrallah  ameongeza kuwa, sababu kuu ya kuiweka harakati ya Hizbullah katika orodha ya makundi ya kigaidi, inatokana na kushindwa Marekani na washirika wake katika kukabiliana na harakati hiyo ambayo kila siku inazidi kuwa na nguvu, irada na uimara wa hali ya juu. Amesisitiza kwamba nchini Lebanon muqawama huo hauungwi mkono tu na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, bali na Walebanon wote ambao wamekuwa wakitoa misaada mingi kwa harakati ya mapambano ya Kiislamu.

3468087

captcha