IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu asema:

Adui mkuu wa taifa la Iran ni Marekani na atapata pigo la kihistoria

6:34 - March 15, 2019
Habari ID: 3471876
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa kwamba adui mkuu wa taifa la Iran ni Marekani na kwamba kamwe taifa hili halitafanya kosa katika kumfahamu adui huyo.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo Alkhamisi ya jana mjini Tehran alipokutana na wajumbe wa Baraza la Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu wa Iran. Katika kikao hicho, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha kwamba adui mkuu wa taifa la Iran ni Marekani na kwamba kamwe taifa hili halitafanya kosa katika kumfahamu adui huyo. Aidha ameongeza kuwa, mfumo wa Kiislamu hauna hautarajii kwamba ipo siku ubeberu wa dunia utasalia kimya mbele ya harakati za kimaendeleo za taifa la Iran. Ameashiria matamshi ya Wamarekani juu ya kuendelezwa mashinikizo na vikwazo dhidi ya taifa la Iran na kusema, Wamarekani katika kukabiliana na Iran wametumia hujuma kubwa na kwamba iwapo taifa hili litajitolea zaidi kwa nyenzo na uwezo wake, basi kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu litaweza kutoa pigo kubwa la kihistoria kwa Marekani.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameashiria kadhia ya namna ya kukabiliana na Marekani na Ulaya na kuongeza kwamba, uzoefu wa Jamhuri ya Kiislamu kuhusiana na Wamarekani na watu wa Ulaya ni mwingi sana,  na kuwa wa hivi karibuni zaidi  unahusiana na mapatano ya nyuklia ya Iran yanaojulikana kamam Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji (JCPOA) na ahadi walizotoa Wamarekani kwamba wangezitekeleza, lakini wakazikengeuka. Amesisitiza kwamba kuna umuhimu wa kutumiwa uzoefu huo katika kukabiliana na Marekani na washirika wake.

Kwingineko katika hotuba yake, Kiongozi Muadhamu amesema katika kukabiliana na hujuma kubwa za maadui ni lazima kuchukuliwe hatua za kujitolea kukubwa kwa nyenzo, uwezo na watu ili kuthibitisha kivitendo imani ya wananchi na viongozi juu ya kukumbuka na kumtegemea Mwenyezi Mungu na kwamba ahadi za Mwenyezi Mungu kuhusu taifa kubwa la Iran zinatimia.

Aidha amesisitiza juu ya udharura wa kupatikana maelewano na uelewa wa kina juu ya 'aina na namna ya kuiongoza nchi na watu walioathirika na changamoto mbalimbali na matukio'. Amesema kwamba, katika masuala ya ndani adui anafanya njama ya kuonyesha kwamba Iran ni dhaifu, huku akionyesha nafasi yake kuwa ni yenye nguvu na iliyo imara, kwa lengo la kuonyesha kuwa nchi hii ina matatizo mengi yasiyoweza kutatuliwa na kwamba hakuna hatua yoyote ya maana iliyochukuliwa katika uwanja huo. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria masuala ya eneo la Magharibi mwa Asia na kusema, ni lazima viongozi wa Iran wafahamu nafasi ya nchi sambamba na kutambua kuwa adui anaendelea kuifuatilia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kwamba, wale wanaokosoa uwepo wa Iran katika eneo sambamba na kueneza propaganda zisizo sahihi, kwa hakika wanamsaidia adui.

3797882

captcha