IQNA

Iran yalaani vikali hujuma za kigaidi misikitini New Zealand, yataka kikao cha dharura cha OIC

15:07 - March 16, 2019
Habari ID: 3471878
TEHRAN (IQNA)-Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vikali hujuma za kigaidi zilizolenga misikiti miwili jana mjini Christchurch New Zealand na kupelekea Waislamu wasiopungua 49 kuuawa shahidi wakiwa katika Sala ya Ijumaa.

Waislamu wengine karibu 50 wamejeruhiwa vibaya katika hujuma hiyo ambayo ilitekelezwa na gaidi raia wa Australia mwenye misimamo mikali ya ubaguzi, Brenton Tarrant, ambaye ni mfuasi sugu wa Rais Donald Trump wa Marekani aliye maarufu kwa misimamo yake dhidi ya Uislamu.

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa ujumbe kufuatia shambulizi hilo la kigaidi nchini New Zialand ambapo sambamba na kulaani vikali hujuma hiyo ya kinyama amesema kuwa, jinai hiyo ya kutisha ni ishara nyingine inayosisitizia umuhimu wa kukabiliana kwa pande zote na ugaidi au chuki zilizoenea dhidi ya wafuasi wa dini fulani, kaumu na kadhalika chuki dhidi ya Uislamu vilivyoshamiri katika nchi za Magharibi.

Baadhi ya serikali za kimagharibi zinahusika

Rais Rouhani amebainisha kwamba ni suala la kusikitisha sana kuona kuwa baadhi ya serikali za Kimagharibi pia zimekuwa zikishiriki katika vitendo hivyo. Rais Hassan Rouhani amezidi kubainisha kwamba, kuenezwa habari zisizo na vigezo na zisizo za kibinaadamu za jinai hiyo ya kigaidi kunakofanywa na baadhi ya vyombo vya habari vya nchi za Magharibi, ni ushahidi mwingine wa ubaguzi wa rangi na kiwango cha hali ya juu cha undumakuwili wao hata kuhusiana na maisha ya wanadamu na kuongeza kuwa, unyama na dhulma hizo za wazi, haziwezi kusahauliwa na wanadamu wenye mwamko na wanaojali thamani  zao. Rais Hassan Rouhani amesema kuwa, jinai ya New Zealand imeonyesha kwamba ugaidi bado ni tatizo sugu duniani na linalohitaji mapambano ya pamoja na pia misimamo isiyokinzana ya nchi zote za dunia katika kukabiliana na ukatili na misimamo ya kufurutu ada katika kila pembe za dunia.

Nchi za Kiislamu zitoe jibu kali

Amesisitiza kwamba jamii ya kimataifa hususan nchi za Kiislamu ni lazima zitoe jibu kali katika kukabiliana na jinai hiyo iliyo dhidi ya binaadamu, sambamba na kuwabaini waungaji mkono waliojificha nyuma ya ukatili huo. Amesema kuwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itafuatilia kwa nguvu zake zote katika ngazi za kimataifa jinai hiyo ili kuhakikisha wahusika na wale waliotoa amri ya kutekelezwa unyama huo wanaadhibiwa. Amebainisha kwamba, Tehran ina imani kwamba umoja na mshikamano wa Waislamu utasaidia kusambaratisha njama hizo za maadui. Kadhalika amesisitiza kwamba, serikali ya Iran imeazimia kwa dhati kupambana na ugaidi na misimamo yote ya ubaguzi wa rangi. Sambamba na kutoa pole kwa familia za wahanga wa shambulio hilo la New Zealand hapo jana ametoa pole pia kwa Waislamu wote duniani na kumuomba Mwenyezi Mungu azilaze roho za mashahidi wa shambulizi hilo la kigaidi mahala pema sambamba na kuwaponya waliojeruhiwa.

Iran yaitisha kikao cha OIC

Wakati huo huo,Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Muhammad Javad Zarif, amefanya mawasiliano na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Mevlüt Çavuşoğlu ambaye ni mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Kiislamu (OIC) ambapo sambamba na kulaani vikali hujuma ya kigaidi na mauaji makubwa dhidi ya Waislamu wa New Zealand, ametaka kutolewa radiamali kali na nchi za Kiislamu kuhusu jinai hiyo ya kutisha.

Katika mawasiliano hayo ya simu, Zarif amesema kuwa, kwa kuzingatia ukubwa wa shambulizi hilo na pia udhalilishaji wa askari wa utawala haramu wa Kizayuni (Israel) dhidi ya misikiti ya Waislamu huko katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Kiislamu (OIC) inatakiwa kuitisha kikao cha dharura na cha haraka katika ngazi ya marais au mawaziri wa mambo ya nje wanachama wa jumuiya hiyo kubwa zaidi ya nchi za Waislamu.

3468141

captcha