Pamoja na hayo, maafisa wa Umoja wa Mataifa wanadai kuwa, yamkini kwa muda wa miaka mingi ijayo, wakimbizi Warohingya hawataweza kurejea nchini Myanmar. Kambi ya wakimbizi Warohingya iliyoko kusini mashariki mwa Bangladesh, ina karibu wakimbizi milioni moja ambayo aghalabu ni Waislamu. Kambi hiyo hivi sasa ni kambi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani. Aghalabu ya watu wa kabila la Rohingya ni Waislamu na kuanzia Agosti mwaka 2017 walianza kukabiliana na mauaji ya kimbari ambayo yamekuwa yakitekelezwa na Jeshi la Myanmar.