IQNA

Uturuki, Pakistan, Malaysia kuanzisha TV ya kukabiliana na chuki dhidi ya Uislamu

11:49 - October 01, 2019
Habari ID: 3472155
TEHRAN (IQNA) – Viongozi wa Uturuki, Pakistan na Malayasia wametangaza azma yao ya kuanzisha televisheni kwa lugha ya Kiingereza kwa lengo ka kukabiliana na wimbi la chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia).

Akizungumza na waandishi habari kuhusu mradi huo, Waziri Mkuu wa Malaysia Mahathir Mohammad amesema: "Tumehisi kuna ripoti nyingi sana kuhusu Uislamu na Waislamu ambazo si sahihi na zilizo kinyume cha mafundisho ya Kiislamu. "

Amesema mradi huo unalenga kuwasilisha taswira sahihi ya Uislamu duniani.

Mapatano kuhusu mpango huo yalifikiwa katika kikao cha pande tatu cha Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan, Waziri Mkuu wa Malaysia Mahathir Mohammad na Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki pembizoni mwa kikao cha 74 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York mwezi Septemba.

Mahathir amesema vyombo vya habari vya kimagharibi hueneza propaganda kuwa Waislamu ni magaidi katika hali ambayo ukweli ni kwamba Uislamu ni dini ya amani. Amesema kwa kuzingatia nukta hizo, "tumehisi kuna haja ya kuwepo jitihada za kueleza uhalisia wa mambo ili Uislamu usituhumiwe kuwa eti ni dini inayounga mkono ugaidi."

Waziri Mkuu wa Pakistan naye amesema kituo hicho cha televisheni kitatengeneza filamu kuhusu historia ya Uislamu kwa lengo la kuwaelimisha Waislamu na wasiokuwa Waislamu.

Katika hotuba yake katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Khan amesema wimbi la chuki dhidi ya Uislamu lilianza baada ya mashambulizi ya Septema 11, 2001 nchini Marekani. Amesisitiza kuwa, ugaidi hauna uhusiano na dini yoyote huku akiongeza kuwa Waislamu sasa wanatengwa na kubaguliwa katika nchi za Magharibi. Ametahadharisha kuwa ubaguzi kama huo utapelekea kuibuka misimamo mikali na hivyo hatua zinapaswa kuchukuliwa.

Kwa upande wake Rais Erdogan akihutubu katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa amesema chuki dhidi ya Uislamu ni hatari sana na kwa msingi huo kuna haka ya kuchukuliw hatua jumuishi ili kukabiliana na hali hiyo.

Amesema kwa kuzingatia kuwa Uturuki uko katika njia inayounganisha ulimwengu wa Mashariki na Magharibi, nchi yake iko tayari kuongoza jitiahda za kukabiliana na chuki dhidi ya Uislamu.

Aidha ametoa wito kwa Umoja wa Mataifa kutangaza Machi 15, siku ambayo misikiti miwili ilihujumiwa huko Christchurch New Zealand, kuwa 'Siku ya Kimataifa ya Mashikamano Dhidi ya Islampohobia'.

3469549

captcha