IQNA

Kesi ya waliomuua kikatili Jamal Khashoggi yaanza Uturuki

12:41 - July 03, 2020
Habari ID: 3472924
TEHRAN (IQNA) - Mahakama moja nchini Uturuki leo imeanza kusikiliza kesi ya maafisa 20 wa utawala wa Saudi Arabia waliohusika na mauaji ya mwandishi wa habari raia wa nchi hiyo Jamal Khashoggi.

Kesi hiyo imeanza kusikilizwa saa nne asubuhi leo kwa wakati wa Uturuki katika mahakama kubwa ya wilaya ya Caglayan iliyoko kwenye mkoa huo wa Instanbul.

Khashoggi, mwandishi wa makala katika gazeti la Washington Post ambaye alikuwa na umri wa miaka 55, aliuliwa ndani ya ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Instanbul Oktoba Pili 2018 baada ya kuingia ubalozini humo alikokwenda kuchukua waraka wa kibali kwa ajili ya mpango wake wa kufunga ndoa.

Maafisa wa Uturuki wanasema mwili wa Khashoggi ulikatwa vipande vipande ndani ya ubalozi huo wa Saudia na watu waliomuua; na mabaki ya kiwiliwili chake hayajapatikana hadi leo.

Mwezi Machi mwaka huu, waendesha mashtaka wa Uturuki waliwafungulia mashtaka raia 20 wa Saudi Arabia kwa kuhusika na mauaji ya Jamal Khashoggi, wakiwemo wasaidizi waandamizi wawili wa zamani wa mrithi wa ufalme wa nchi hiyo Mohammad bin Salman, ambaye kiuhalisia ndiye mtawala wa nchi hiyo hivi sasa.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, naibu mkuu wa zamani wa idara ya intelijensia ya Saudi Arabia Ahmed al-Assiri anakabiliwa na shtaka la kuunda kikosi cha mauaji na kupanga mauaji ya mwandishi huyo wa habari aliyekuwa mkosoaji mkubwa wa utawala wa Aal Saud.

Mshauri wa zamani wa mahakama ya kifalme na masuala ya vyombo vya habari Saud al-Qahtani, yeye ameshtakiwa kwa kuchochea na kuongoza operesheni kwa kutoa amri na maagizo kwa kikosi hicho cha mauaji.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya mauaji ya Jamal Khashoggi ni maafisa wa Saudia ambao wanadaiwa kushiriki katika utekelezaji wa operesheni ya mauaji hayo. Waendesha mashtaka wa Uturuki wameshatoa waranti wa kukamatwa washtakiwa hao.

3908315

captcha