IQNA

Suu Kyi aliyeshirikiana na jeshi kuwakandamiza Waislamu ashtakiwa na jeshi hilo hilo

20:24 - February 03, 2021
Habari ID: 3473618
TEHRAN (IQNA) - Jeshi la Myanmar lilivyofanya mapinduzi na kutwaa madaraka ya nchi limetangaza kuwa, lina mpango wa kumfungulia mashtaka ya uhaini Aung San Suu Kyi kiongozi wa chama tawala cha nchi hiyo cha NLD na viongozi wengine kadhaa wa nchi hiyo.

Mbali na Suu Kyi ambaye hadi kukamatwa kwake alikuwa waziri wa mambo ya nje, wanasiasa na wabunge kadhaa wa chama chake nao wanakakabiliwa na mashtaka ya uhaini.

Kwa mujibu wa sheria za Myanmar endapo watapatikana na hatia watakabiliwa na kifungo cha hadi miaka 20 jela au hata adhabu ya kifo.

Jeshi linaonekana kumgeuka Suu Kyi ambaye amekuwa akiliunga mkono katika kuwakandamiza na kuwaua kwa umati Waislamu wa jamii la Rohingya. Tokea mwaka wa 2017, Suu Kyi ameshirikiana na jeshi hilo hilo kuwakandamiza na kuwaangamiza kwa umati Waislamu wa jamii ya Rohingya katika jimbo la Rakhine. Zaidi ya Waislamu milioni moja wa eneo hilo wamelazimika kukimbilia nchi jirani ya Bangladesha wakihofia maisha yao. Suu Kyi alilitetea jeshi katika  hatua zake za ukandamizaji Waislamu lakini sasa jeshi hilo limemgeuka.

Mnamo Mosi Februari, Jeshi la Myanmar lilitangaza kudhibiti madaraka ya nchi baada ya kumkamata Rais wa nchi na viongozi wengine akiwemo Aung San Suu Kyi, kiongozi wa chama tawala mwenye ushawishi nchini Myanmar, kufuatia siku kadhaa za mivutano nchini humo ambayo ilizua hofu ya kutokea mapinduzi.

Kisingizio cha jeshi cha kufanya mapinduzi hayo ni madai ya kutokea wizi na udanganyifu katika zoezi la uchaguzi wa Bunge wa Novemba 2020, ambapo, chama tawala cha National League for Democracy (NLD) kinachoongozwa na Aung San Suu Kyi kiliibuka na ushindi.

Baada ya chama tawala cha NLD kudai kwamba, kimepata ushindi wa asilimia 83 wa viti vya Bunge, jeshi la Myanmar liliibuka na kukituhumu chama hicho kwamba, kimefanya udanganyifu na kuchakachua matokeo ya uchaguzi huo na kuitaka Tume ya Uchaguzi kushughulikia madai hayo. Hata hivyo Tume ya Uchaguzi ya Myanmar ilitupilia mbali madai hayo ya jeshi na kueleza kwamba, uchaguzi huo ulikuwa salama.

Kwa mujibu wa Katiba ya Myanmar, asilimia 25 ya viti vya Bunge ni vya jeshi la nchi, kama ambavyo jeshi la nchi hiyo lina haki ya kikatiba ya kutangaza majina matatu kwa ajili ya nafasi za wizara.

Baada ya kutangaza hali ya hatari ya mwaka mmoja,  jeshi la Myanmar lilitoa pia orodha ya majina 11 ya shakhsia watakaoongoza kipindi cha mpito cha mwaka mmoja na kwamba, uchaguzi mpya wa Bunge utafanyika baada ya kipindi hicho.

Wakati huo huo mwenyekiti wa Baraza kuu la umoja wa Mataifa Volkan Bozkir amebainisha wasi wasi wake kuhusu hali ya Waislamu Warohingya nchini Myanmar baada ya mapindzi ya kijeshi. Amesema yamkini jeshi likazidisha ukandamizaji wa Waislamu nchini humo.

395158

captcha