Tutaendelea kuishukuru neema hii kwa kuikariri aya ya 43 ya Suratul A'araf isemayo:" Alhamdulillah! Kuhimidiwa ni kwa Mwenyezi Mungu, ambaye aliye tuhidi kufikia haya. Wala hatukuwa wenye kuhidika wenyewe ingeli kuwa Mwenyezi Mungu hakutuhidi.
Hakika Mitume wa Mola wetu Mlezi walileta Haki. Katika kuonyesha
ushukurivu wetu kwa neema ya Idul-Ghadir, tunamshukuru Mwenyezi Mungu na
tunakukaribisheni wapenzi wasikilizaji kusikiliza kipindi hiki maalumu
tulichokuandalieni kwa mnasaba huo.
Katika kipindi cha miaka 23, Bwana Mtume SAW alisumbuka na kufanya jitihada
kubwa mno hadi kuuwezesha kuchipua na kustawi mmea mchanga wa dini tukufu ya
Uislamu. Katika muda wote huo alivumilia mateso, machungu na misukosuko mingi
na hakufanya ajizi hata kwa lahadha ndogo katika kutekeleza jukumu na wajibu
wake wa kufikisha risala na wito wa Mola wake.
Katika mwaka wa kumi Hijria, ujumbe kutoka ulimwengu wa ghaibu ulimfikia kumjulisha kwamba muda si mrefu ataondoka katika ulimwengu huu. Kwa hivyo akafanya juhudi za mtawalia kuhakikisha anatekeleza kwa ukamilifu kila lile lenye ulazima kwa ajili ya utukukaji wa dini ya Uislamu na lenye maslaha kwa Waislamu. Suala la Ukhalifa na uongozi baada yake ni moja ya mambo muhimu zaidi yaliyokuwa yakimshughulisha Bwana Mtume Muhammad SAW. Kwa sababu yeye ni Mtume wa mwisho wa Mwenyezi Mungu na baada yake yeye hatokuja Mtume mwengine atakayetumwa na Yeye Mola. Kwa hiyo mtu ambaye atabeba jukumu la utawala na uongozi wa watu baada yake anapaswa awe mja mtiifu kwa Allah, dhihirisho la ukamilifu wa utu na aliyeepukana na kila aina ya upotofu ili awe na ustahili wa kuuongoza umma baada ya Bwana Mtume. Kwa sababu hiyo katika Hija yake ya mwisho iliyojulikana pia kama Hijjatul-Wida'a, Bwana Mtume Muhammad SAW alimtangaza rasmi kwa Waislamu wote kiongozi wa umma baada yake.
Tukio la kutambulishwa khalifa wa Bwana Mtume katika Hija yake ya kuaga
limeelezewa katika vitabu na maandiko ya historia kama ifuatavyo: Baada ya
kumalizika utekelezaji wa amali za Hija Bwana Mtume SAW alianza safari ya
kuelekea Madina. Wakati alipofika eneo la Raabigh katika mahali paitwapo Ghadir
Khum, Jibril mwaminifu alimteremkia na kumfikishia ujumbe unatoka kwa Mwenyezi
Mungu usemao:" Ewe Mtume! Fikisha uliyo teremshiwa kutoka kwa Mola wako
Mlezi". Bwana Mtume ambaye alikuwa akielewa unafiki wa baadhi ya watu, na
akawa na wasiwasi juu ya mustakabali wa umma wa Kiislamu, alitaamali kidogo.
Katika lahadha hiyo Jibril mwaminifu aliteremka ardhini kwa mara ya pili na
kumsomea Bwana Mtume sehemu inayofuata ya aya inayosema: "Na ikiwa
hukufanya hayo basi hukufikisha ujumbe wake." Bwana Mtume alikuwa
akitafakari ni vipi aufikishe ujumbe huo, malaika Jibrili akamteremkia kwa mara
nyengine tena na ujumbe wa Allah usemao:" Na Mwenyezi Mungu atakulinda na
watu. Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi watu makafiri." Hapa linajitokeza
swali hili, kwamba ujumbe huo ni muhimu kiasi gani ikiwa hautofikishwa kwa
watu, Bwana Mtume atakuwa kwa kweli hajafikisha risala ya Mola wake? Ni nukta
gani muhimu ambayo lazima ielezwe na ambayo kwa ajili ya kufikishwa kwake
Mwenyezi Mungu anamtoa wasiwasi Mtume wake mtukufu na kumpa hakikisho kuwa
atamlinda na madhara ya watu? Bila ya shaka makusudio ya madhara ya watu si
madhara ya kumdhuru kimwili au kimali n.k, kwa sababu Bwana Mtume alikuwa
shujaa zaidi ya watu wote, kwani hakuwahi hata mara moja kuingiwa na chembe ya
hofu katika medani za vita na wakati mapigano yalipokuwa yameshtadi na kupamba
moto. Hofu aliyokuwa nayo mtukufu huyo ilikuwa ni ya kuchelea madhara kwa asili
ya dini yenyewe yatakayosababishwa na baadhi ya watu waliokuwa wamezongwa na
ujahili na hali ya unafiki. Ili kutekeleza amri hiyo ya Mwenyezi Mungu, na
licha ya joto kali lenye kuunguza na lisiloweza kuhimilika la Ghadir Khum,
Bwana Mtume alitoa amri msafara wa mahujaji usimame mahala hapo. Wakati umati
mkubwa wa watu ulipokuwa umejumuika hapo Bwana Mtume SAW alipanda juu ya mahali
palipoinuka, na baada ya kumhimidi na kumshukuru Mwenyezi Mungu alisema: Hadi
wakati huu Jibrili amesha nishukia mara tatu na kunipa amri kutoka kwa Mwenyezi
Mungu ya kunitaka nisimame katika ardhi hii na kuhitimisha ufikishaji wa risala
yake.
Je mimi si bora zaidi kwenu kuliko nafsi zenu wenyewe? Wote wakajibu kwa kusema: Ndiyo. Bwana Mtume akaendelea kuwauliza: Je mimi si Mtume na kiongozi wenu? Wote kwa pamoja wakayathibitisha maneno hayo. Baada ya hapo akaushika mkono wa Ali bin Abi Talib, akauinua juu na kusema:"Yule ambaye mimi namtawalia mambo yake, basi huyu Ali anamtawalia mambo yake". Waandishi wa historia wameandika kuwa watu waliokuwa wamehudhuria mahala hapo walikuwa ni baina ya elfu 80 hadi laki moja na ishirini. Baada ya tukio hilo ndipo ilipoteremshwa aya ya tatu ya Suratul Maida isemayo:" Leo walio kufuru wamekata tamaa na Dini yenu; basi msiwaogope, bali niogopeni Mimi. Leo nimekukamilishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni UISLAMU uwe ndiyo Dini. Tukio hilo muhimu liliwafanya makafiri wakate tamaa. Watu ambao walikuwa wakingojea Bwana Mtume afariki dunia ili kwa kukosekana kiongozi atokanaye na uteuzi wa Mola waweze kutekeleza malengo yao maovu. Lakini katika tukio la Ghadir Khum, kwa kutangazwa ukhalifa wa Ali (AS), ambaye kama alivyokuwa Bwana Mtume, alikuwa amepambika kwa sifa za ushujaa, umaizi, subira na uthabiti, tamu ya matumaini waliyokuwa nayo makafiri iligeuka kuwa shubiri. Tukio hili adhimu lilionyesha kuwa kwa mtazamo wa Uislamu, mtawala na kiongozi wa umma wa Kiislamu anapaswa awe mtu mwema, mweledi, mudiri, mjuzi na mwenye uchungu wa dini; na si kila mtu anaweza kuteuliwa kushika wadhifu huo muhimu.
Suala la ukhalifa na uongozi baada ya Mtume wa mwisho wa Allah lilikuwa na
umuhimu mkubwa mno kiasi kwamba hata kabla ya tukio la Ghadir Khum, lilishawahi
kuashiriwa na Bwana Mtume katika nyakati na minasaba tofauti. Kwa hakika tokea
alipopewa jukumu na Mola la kuwatangazia na kuwalingania Uislamu jamaa zake wa
karibu Bwana Mtume SAW alilizungumzia suala la khalifa baada yake. Baada ya
kuwalingania jamaa na watu wake hao wa karibu Bwana Mtume aliwaambia:"Enyi
wana wa Abdulmuttalib, naapa kwa Mwenyezi Mungu simjui mtu yeyote miongoni mwa
Waarabu ambaye ameieletea kaumu yake kitu bora kuliko kile ambacho mimi
nimekeuleteeni nyinyi. Si kinginecho nilichokuleteeni ila ni kheri ya dunia na
akhera, na Mwenyezi Mungu ameniamrisha nikulinganieni jambo hilo. Basi yeyote
kati yenu atakayenisaidia katika jambo hilo atakuwa ndugu yangu, wasii wangu na
khalifa wangu juu yenu." Katika hadhara ile ile Ali bin Abi Talib, pamoja
na kwamba alikuwa kijana chipukizi alionyesha uaminifu na kujitolea kwake nafsi
yake kwa ajili ya Bwana Mtume, akasema kuwa atamsaidia mtukufu huyo katika
utekelezaji wa jukumu alililopewa na Mola. Na kwa hivyo katika majlisi na
hadhara hiyo akatambulishwa kuwa khalifa wa Mtume wa Allah. Baada ya hapo pia
katika kipindi kilichofuatia cha miaka ya baada ya hijra ya Bwana Mtume kuhamia
Madina, suala la ukhalifa wa Ali (AS) baada ya Mtume lilikaririwa na Bwana
Mtume kwa kiwango ambacho takribani watu wote wa Madina walikuwa na uelewa wa
suala la ukhalifa wa Ali (AS).
Tukio la Ghadir ni tukio mashuhuri mno, na hakuna mtu yeyote awezaye
kukadhibisha kujiri kwa tukio hilo muhimu la kihistoria. Sayyid Murtadha Alamal
Huda, mwanazuoni mkubwa wa Ulimwengu wa Kiislamu ameandika kuhusiana na suala
hili kwa kusema:"Mtu atakayetaka ushahidi wa ukweli wa habari hii ni sawa
na mtu anayetaka ushahidi wa ukweli wa habari ya vita na matukio maarufu
yaliyotokea katika maisha ya Mtume wa Mwenyezi Mungu; na ni sawa na kusema
kwamba anatilia shaka tukio lenyewe la Hijjatul-wida'a, kwa sababu yote hayo
mawili yana umashuhuri wa kiwango kimoja". Maulamaa wakubwa wa Ahlu
Sunnah, nao pia wameinakili hadithi ya tukio la Ghadir Khum kwa sanadi na
mapokezi tofauti. Kwa kutoa mfano, Imam Ahmad bin Hanbal, mmoja wa maimamu wa
madhehebu nne za Kisuni amemnukuu katika kitabu chake kiitwacho Al Musnad mmoja
wa masahaba wa Mtume aitwaye Zaid bin Arqam akisema:"Tulikuwa
tumekusanyika pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu katika bonde liitwalo bonde la
Khum, kisha akatoa amri ya kusali. Hapo tukasali Sala ya Adhuhuri pamoja na
mtukufu huyo, kisha akasoma khutba; na katika hali ambayo kitambaa kilikuwa
kimetundikwa juu ya mti ili aweze kuwa kivulini na kutopigwa sana na mwanga wa
joto la jua lenye kuunguza, Bwana Mtume alisema: Je hamjui? Je hamshuhudii kuwa
mimi ni bora zaidi kwa kila muumini kuliko nafsi yake mwenyewe? Wote wakasema:
Ndiyo! Akasema: Kila yule ambaye mimi ninamtawalia mambo yake, huyu Ali
anamtawalia mambo yake, Ewe Mola mpende kila mwenye kumpenda na mfanye adui
kila mwenye kumfanyia uadui".
Hakim Naishaburi, naye pia amenukuu kutoka kwenye vitabu viwili vya maulamaa
wakubwa wa Kisuni Bukhari na Muslim ya kwamba:"Wakati Mtume wa Allah
alipokuwa anarejea kutoka kwenye Hijjatul-Wida'a alisimama Ghadir Khum na kutoa
amri watu wakusanyike chini ya miti. Kisha akasema: Karibuni hivi Mola wangu
ataniita na mimi nitaitika wito.
Nimekuachieni vitu viwili vyenye thamani kubwa ambapo kimoja ni kikubwa
zaidi ya kingine: Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu, basi angalieni
mtaamiliana navyo vipi baada yangu. Hakika viwili hivi havitengani abadani hadi
vitakapoingia kwangu katika hodhi". Kisha akasema, Mwenyezi Mungu Azza wa
Jalla ni mwenye kunitawalia mimi mambo yangu, na mimi ni mwenye kumtawalia kila
muumini mambo yake. Kisha akaushika mkono wa Ali na kusema: Kila ninayemtawalia
mambo yake, basi huyu Ali anamtawalia mambo yake. Ewe Mola! Mpende
atakayeikubali Wilaya yake na mfanye adui kila atakayemfanyia uadui".
Maulamaa wengine wengi wa Kisuni kama Tirmidhi, Ibnu Majah, Ibn Asaakir, Ibn
Naiim, Ibn Athir, Kharazmi, Suyuti, Ibn Hajar, Haithami, Ghazali pamoja na
Bukhari wamelitaja tukio la Ghadir katika vitabu vyao. Abu Sa'ad Mas'uud bin
Nasir Sajistani, mmoja wa maulamaa wa Kisuni ameeleza katika kitabu chake
kiitwacho Ad Dirayah fii Hadithil Wilayah kuwa ameinukuu hadithi hii kutoka kwa
masahaba 120 wa Bwana Mtume. Kwa hivyo sanadi ya hadithi ya Ghadir ni madhubuti
na ya yakini kwa kiasi ambacho hakuna mtu anayeweza kuikana na kuficha uhakika
wake. Abdulfatah Abdul Maqsud, mwandishi na mhakiki wa Kimisri ameeleza haya
katika kitabu chake alichoandika kuhusu Imam Ali (AS):" Hadithi ya Ghadir,
bila ya shaka yoyote ni hakika isiyoweza kubatilishwa, inga'rayo na kuangaza
mithili ya mwanga wa mchana".