IQNA

Baraza la Haki za Binadamu la UN kujadili hujuma dhidi ya Qur'ani

14:18 - September 12, 2023
Habari ID: 3477587
Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa linatazamiwa kufanya kikao hivi karibuni cha kujadili vitendo vya mara kwa mara vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu katika nchi za Magharibi.

Volker Turk, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa alisema hayo jana Jumatatu mjini Geneva katika ufunguzi wa kikao cha 54 cha Baraza la Haki za Binadamu la UN na kuongeza kuwa, mkutano huo wa kujadili kwa kina ongezeko la vitendo vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu utafanyika Oktoba 6.

Turk ameeleza bayana kuwa, "Badala ya dunia kushuhudia umoja wenye dhamira na ushirikiano katika uongozi, inashuhudia siasa za migawanyiko, mifarakano na uharibifu.

Afisa huyo wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa amesema wimbi la karibuni la matukio 30 ya kuchomwa moto Qur'ani linaenda sambamba na azma ya baadhi ya watu kutaka kuibua mifarakano katika jamii na baina ya nchi tofauti.

Hivi karibuni, Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alimuandikia barua Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, akimtaka achukue msimamo mkali dhidi ya vitendo hivyo vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu.

Ulimwengu wa Kiislamu umelaani vikali wimbi hilo la vitendo viovu vya kuvunjiwa heshima Kitabu hicho Kitukufu cha Waislamu zaidi ya bilioni moja hasa katika nchi za Sweden na Denmark kwa ridhaa ya serikali za nchi hizo za Magharibi.

 

captcha