IQNA

Kiongozi Muadhamu azitaka nchi za Kiislamu kushikamana kukabiliana na mabeberu

21:47 - October 03, 2023
Habari ID: 3477686
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, baada ya madola ya kiistikbari na kibeberu kuhisi hatari kutokana na kuenea nguvu za mafundisho ya Qur'ani Tukufu, yameamua kuendesha kampeni za kukivunjia heshima Kitabu hicho Kitakatifu cha Mwenyezi Mungu.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo leo Jumanne hapa Tehran wakati alipoonana na viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu, mabalozi wa nchi za Kiislamu, wageni wa Mkutano wa Umoja wa Kiislamu na wananchi wa matabaka tofauti kwa mnasaba wa maadhimisho ya Maulid ya Bwana Mtume Muhammad SAW na Imam Sadiq AS na kusisitizia haja ya kushikamana nchi za Kiislamu na kuwa na msimamo mmoja katika masuala yao ya kimsingi kwa ajili ya kupambana na uistikbari wa Marekani na madola mengine ya kibeberu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kisilamu pia amesema, ulimi wa mwanadamu hauna uwezo wa kutaja vilivyo fadhila na utukufu wa Mtume Muhammad SAW akisisitiza kuwa, jua linaloangaza la nuru ya Bwana Mtume Muhammad SAW linamfanya kila mwanadamu kuwa na deni kwake kwani Bwana Mtume ni mithili ya daktari bingwa na mahiri sana ambaye ana elimu na maarifa makubwa ya kutibu magonjwa yote yakiwemo ya umaskini, ujinga, dhulma, ubaguzi, kuabudu hawa za nafsi, ukosefu wa imani, kufanya mambo kiholela, ufisadi wa kimaadili na madhara yake katika jamii n.k.

Amesema ndoto za kuweza kukidhoofisha Kitabu Kitukufu cha Qur'ani kwa kukivunjia heshima kiupumbavu, inazidi kuwafedhehesha maadui na kufichua njama zao zilizjificha.

Amesisitiza kwa kusema: Qur'ani ni Kitabu cha hikma na maarifa, ni Kitabu cha kumjenga mwanadamu na kumwamsha, hivyo kuifanyia uadui Qur'ani Tukufu kwa hakika ni kufanyia uadui mafundisho aali na matukufu kabisa.

Katika sehemu nyingine ya miongozo yake ya busara, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amegusia Wiki ya Umoja na kuwakhutubu viongozi na wanasiasa wa nchi za Kiislamu, wanafikra na watu wenye vipaji wa Ulimwenu wa Kiislamu akiwaambia kuwa, kuna udharura wa kuzingatia swali hili kwamba, ni nani hasa anayeufanyia uadui umoja na mshikamano wa nchi za Kiislamu na Waislamu. Ni nani wanaopata madhara unapokuwepo umoja huo? Na ni mikono ya akina nani itakatwa ili isiweze kupora na kuingilia masuala ya nchi za Kiislamu, iwapo Waislamu wataungana?

Amesema, kushikamana nchi za Kisilamu za eneo la Asia Magharibi na Afrika Kaskazini kutakata mikono ya wizi na ubeberu ya madola ya kiistikbari kama Marekani akisisitiza kuwa, leo hii Marekani imepata pigo la kisiasa na kiuchumi kutoka kwa nchi za eneo hili na imeamua kupora waziwazi utajiri wa mafuta wa Syria, inawahifadhi na kuwapa mafunzo magaidi makatili kama wa Daesh na kuwatumia kuingilia masuala ya Waislamu. Lakini kama nchi zote zitaungana na iwapo nchi kama za Iran, Iraq, Syria, Lebanon, Saudia, Misri, Jordan na nchi zinazopakana na Ghuba ya Uajemi zitakuwa na msimamo mmoja, basi madola ya kibeberu hayatothubutu kuingilia masuala ya nchi hizo na ya Ulimwengu wa Kiislamu.

parstoday

captcha