IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Madola ya Magharibi yanamdhulumu mwanamke na kukanyaga hadhi na utu wake

20:05 - January 04, 2023
Habari ID: 3476358
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutaja msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu mkabala wa wanaodai kinafiki kuwa wanatetea haki za wanawake wa Kimagharibi kuwa ni wa kudai na kuhujumu na akasema kuwa, Magharibi ya kisasa na utamaduni ulioporomoka wa Magharibi vina hatia katika suala hili na wametenda makosa na uhalifu dhidi ya utu na hadhi ya mwanamke.

Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo Jumatano katika mkutano na na kundi la wanawake wasomi katika hotuba yake ya kabla ya sherehe za kuadhimiza siku ya kuliza Bibi Fatima al Zahra (SAW) na Siku ya Wanawake hapa nchini Iran . Akizungumza katika hadhara hiyo ya wanawake wasomi na wanaharakati wa masuala ya kiutamaduni, kijamii na kielimu, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, medani ya kazi na kumtazama mwanamke kama chombo cha kushibisha matamanio ya mwanaume ni dhulma mbili za kimsingi dhidi ya wanawake katika nchi za Magharibi na kuongeza kuwa, lengo kuu la kuibua suala la uhuru wa wanawake katika nchi za Magharibi ni kuwaondoa nyumbani na kuwapeleka viwandani ili kuwatumia kama nguvu kazi nafuu na ya bei rahisi.

Ayatullah Khamenei amesema kuwa: "Katika mtazamo wa ubepari wa Magharibi, wanaume wana kipaumbele juu ya wanawake kwa sababu mtaji na uwezo wa kifedha huainisha nafasi na hadhi za watu, na mwanaume amekuwa msimamizi wa masuala ya kiuchumi na kibiashara. Suala la uhuru wa wanawake liliibuliwa katika nchi za Magharibi kwa shabaha ya kuwatumia katika viwanda mkabala wa kupewa mishahara dunia na ya chini. Katika mfumo wa kibepari, mtaji huwa na thamani na nafasi ya juu zaidi kuliko ubinadamu. Ubinadamu wa watu unahudumia mtaji, na kila mtu anayeweza kuzalisha na kukusanya mali zaidi huwa na thamani na hadhi kubwa zaidi."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Kwa mujibu wa mtazamo huu wa ubepari, wanaume huwa bora na juu kuliko wanawake, na mshahara wa wanawake hivi sasa kwa kazi sawa na zile zinazofanywa na wanaume, ni duni kuliko wa wanaume katika nchi nyingi za Magharibi.

Ameashiria takwimu na uhakika unaotangazwa hata na vituo rasmi vya nchi za Magharibi na kusema, madai ya nchi za Magharibi eti ya kutetea haki za wanawake ni jeuri kubwa. Amesema uhuru unaodaiwa katika mfumo wa kibepari ni sawa na “kumteka na kumtusi” mwanawake, na mwanadamu anaona aibu hata kutaja baadhi ya matukio yaliyojiri katika nchi za Magharibi kuhusiana na wanawake.

Ayatullah Khamenei ameitaja hali ya familia katika nchi za Magharibi kuwa imesambaratika na akasema kwamba, hatari hiyo pia imewalazimisha wanafikra wanaopenda kheri wa Kimagharibi na wanamageuzi kupaza juu sauti zao za upinzani, lakini mporomoko wa familia huko Magharibi umekwenda kwa kasi kubwa sana kiasi kwamba haiwezekani kuusimamisha au kuurekebishwa.

Ayatullah Ali Khamenei pia ameashiria njama nyingi zinazofanywa katika siku za hivi karibuni dhidi ya vazi la hijabu na kuhoji kwamba, ni watu gani waliosimama kukabiliana na njama hiyo? Ni wanawake wenyewe tena katika hali ambayo wale wasiolitakia mema taifa walikuwa wakitarajia kwamba wanawake wasio na vazi kamili la hijabu watatupilia mbali hijabu zao, lakini wanawake hawakufanya hivyo, na badala yake wametoa pigo kali kwa wendeshaji na watangazaji wa njama hiyo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, vazi la hijabu ni sharia ya lazima isiyoweza kukiukwa.

Ayatullah Khamenei amezitaja huduma za Jamhuri ya Kiislamu kwa wanawake kuwa ni miongoni mwa vipengee muhimu ambavyo haviwezi kusahaulika na kuongeza kuwa: Kabla ya ushindi wa Mpinduzi ya Kiislamu hapa nchini, idadi ya wanawake wanasayansi na wabobezi katika watafiti ilikuwa ikihisabiwa kwa vidole, lakini mapinduzi hayo yamezidisha idadi ya wanawake wasomi kiasi kwamba wanafunzi wa kike wamezidi idadi ya wanafunzi wa kiume katika vyuo vikuu vya Iran katika baadhi ya miaka, na idadi kubwa ya wanawake wanafanya kazi mbalimbali katika nyanja za sayansi na teknolojia.

4112059

captcha