IQNA

Khatibu wa Sala ya Ijumaa Tehran

Wanaochoma moto Qur'ani Tukufu kimsingi wanajichoma moto wao wenyewe

19:26 - August 04, 2023
Habari ID: 3477381
TEHRAN (IQNA)- Khatibu wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran ameeleza kuwa, wale wanaochoma moto nakala za Qur’ani Tukufu kwa hakika wanajichoma moto wao wenyewe na kusema: Si jambo rahisi kwa kila mtu kujua hakika ya Qur’ani ambayo ni roho na rehema ya Mwenyezi Mungu, na kufanya ukaidi dhidi ya neno la Mungu ni ishara ya roho ya kishetani.

Hujjatul-Islam Kazem Seddiqi, khatibu wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran ameashiria watu wanaochoma moto nakala za Qur'ani katika baadhi ya nchi za Ulaya na kusema: "Hawa viumbe waovu wanaoichoma moto Qur'ani Tukufu hawana njia ya kuifikia na kuifahamu Qur'ani na kwa hakika wanajichoma moto wao wenyewe."

Hujjatul-Islam Kazem Seddiqi amesema kuwa uchamungu ndio njia ya uokovu, na ukosefu wa uchamungu ndio sababu ya kuangamia na kuongeza kuwa: “Uchamungu ni nyumba imara, na mtu anayeishi katika ngome hii atasalimika na shari ya nafsi inayoamrisha maovu na yenye kiburi; lakini kinyume chake, ukosefu wa taqwa na uchamungu huwa sababu ya kuangamia kwa mwanadamu.

Vitendo viovu vya kuvunjia heshima kitabu kitukufu cha Qur'ani Tukufu vimelaaniwa na jamii ya kimataifa akiwemo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ambaye ametangaza mshikamano wake na jamii ya Waislamu na kulaani hatua yoyote ya hujuma na propaganda chafu dhidi ya Uislamu na inayochochea mivutano.

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis pia amelaani vitendo vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu katika nchi za Uswidi na Denmark na kusisitiza kuwa, vitendo hivyo vya kudhalilisha matukufu ya kidini havina tofauti na ukatili.

Habari zinazohusiana
captcha