IQNA

Rais Tebboune: Utawala wa Israel umevuruga uhusiano wa Algeria na Morocco

22:51 - February 17, 2022
Habari ID: 3474939
TEHRAN (IQNA)- Rais Abdelmadjid Tebboune wa Algeria amesema utawala wa Kizayuni wa Israel ndio chanzo cha kuvurugika uhusiano wa nchi yake na Morocco.

Katika mahojiano na televisheni ya kitaifa ya Algeria, Rais Tebboune amesema, kuwa Israel na Morocco zinafanya njama ya kuibua hitilafu kati ya Ofisi ya Rais na Jeshi la Algeria na kuzusha fitna nchini humo.

Aidha amesema kwamba, Morocco na utawala wa Kizayuni wa Israel ndio wanaoendesha njama za kuzusha fitina na kueneza habari za uongo nchini Algeria.

Rais Abdelmadjid Tebboune amesema kuwa, Morocco inatumia vyombo vya propaganda kwa ajili ya kusambaza habari za uongo, kutoa pigo kwa umoja wa kitaifa na kulidhalilisha jeshi la Algeria na kwamba Israel inaihami na kuiunga mkono Morocco katika suala hilo.  

Algeria imekuwa mstari wa mbele kupinga hatua ya baadhi ya nchi za Kiarabu ikiwemo Morocco ya kuanzisha uhusiano rasmi na wa wazi wa kidiplomasia na utawala haramu wa Israel. Mwishoni mwa mwaka 2020 pia Algeria ilikata uhusiano wake na nchi jirani ya Morocco baada ya Rabat kuanzisha uhusiano rasmi na utawala haramu wa Israel, na kutokana na ujasusi wa Morocco nchini Algeria kwa kutumia programu ya kijasusi ya Israel ya Pegasus. 

Vilevile Algeria iliongoza juhudi za nchi kadhaa za Afrika zilizofanikisha kusimamishwa nafasi ya utawala wa Kizayuni kama mwanachama mwangalizi katika Umoja wa Afrika.

4036922

Kishikizo: algeria morocco israel
captcha