Katibu mkuu wa OIC Iyad Madani amesema ofisi yake inawasiliana na nchi wanachama kwa lengo la kuitisha kikao pembizoni mwa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York baadaye mwezi huu.
Amesisitiza kuwa mutano huo ni muhimu na wa dharura kwa kuzingatia hujuma zisizo na kikomo dhidi ya Msikti wa Al Aqsa na njama za kuugawa msikiti huo.
Wachambuzi wa mambo wanaamini kwamba, Baytul Muqaddas na Msikiti wa al-Aqswa sasa vinakabiliwa na duru mpya ya vitisho na njama za utawala wa Kizayuni wa Israel ambapo moja ya njama hizo ni mpango mchafu wa utawala huo ghasibu wa kutaka kuugawa msikiti huo katika sehemu mbili za Wapalestina na Wazayuni na kugawa pia nyakati za kuingia na kutoka katika msikiti huo. Katika mazingira kama haya ya njama mtawalia za Wazayuni maghasibu dhidi ya msikiti wa al-Aqswa, bila shaka kuna udharura kwa Wapalestina, Waislamu na jamii ya kimataifa kuonyesha radimali zao za kukabiliana na njama hizo za Wazayuni za kila siku iendayo kwa Mungu.
Masjidul Aqsa ni kibla cha kwanza cha Waislamu na eneo la tatu kwa utukufu baada ya Masjidul Haram mjini Makka na Masjidun Nabawi mjini Madina huko Saudi Arabia.