IQNA

Muungano usio na maana na wa kimaonyesho wa Saudia dhidi ya ISIS

21:32 - December 17, 2015
Habari ID: 3464302
Saudi Arabia na nchi kadhaa ambazo ni waungaji mkono wa wazi wa ugaidi zimeunda kile kinachodaiwa kuwa eti ni 'muungano dhidi ya ugaidi'.

Gazeti la Washington Post la Marekani limeandika makala na kusema muungano huo hauna maana.

Nalo gazeti la Quds la mjini Tehran, leo katika tahariri yake limeandika kuwa: "Saudi Arabia na baadhi ya nchi za Kiarabu katika eneo la Mashariki ya Kati zimeunda muungano mpya wa kile zinachodai kuwa ni vita dhidi ya ugaidi katika eneo hilo."

Gazeti hilo limeandika kuwa, waungaji mkono wakuu wa Daesh, al-Qaeda na Boko Haram wako katika muungano huo unaoongozwa na Saudia.

Gazeti la Quds limeendelea kuandika kuwa, Saudi Arabia haijaweza kufikia malengo yake haramu katika muungano mwingine wa kimaonyesho dhidi ya ugaidi unaongozwa na Marekani na hivyo wakuu wa Riyadh wameamua kuunda muungano wanaouongoza binafsi.

Gazeti la Quds limeandika kuwa, "ni kichekesho kikubwa kuona Saudi Arabia ikisema iko tayari kutuma wanajeshi kukabiliana na makundi ya kigaidi katika hali ambayo ni Saudia yenyewe iliyowapa mafunzo na silaha magaidi hao."

Mhariri wa gazeti la Quds anasema lengo la watawala wa Saudia katika kuunda muungano huo bandia ni kujaribu kujikwamua kutoka katika kinamasi walichotumbukia ndani yake katika vita vya Yemen.

Siku ya Jumanne, Saudi Arabia ilitangaza muungano unaojumuisha nchi 34 za Waislamu eti kwa lengo la kupambana na ugaidi. Muungano huo unajumuisha nchi za Kiarabu katika Ghuba ya Uajemi, nchi kadhaa za Asia na Afrika. Nchi kama vile Pakistan, Malaysia na Indonesia zimeshatangaza kupinga muungano wa kijeshi na Saudia na kusema hazikushauriwa wakati wa kuundwa muungano huo. Saudi imeunda muungano huo unaojumuisha nchi zinazokumbwa na vita kama vile Somalia, Libya pamoja na nchi iliyofilisika ya Chad na pia Visiwa vya Comoro vyenye jeshi la kitaifa lenye wanajeshi 500 tu. Nchi muhimu katika vita dhidi ya ugaidi kama vile Iraq, Iran na Syria hazikualikwa katika muungano huo.

3464149

captcha