IQNA

Mawaidha

Nukta nne kuhusu Usiku wa Qadr

14:17 - April 09, 2023
Habari ID: 3476840
TEHRAN (IQNA) – Kwa mujibu wa aya za Qur’ani Tukufu, Usiku wa Qadr au Laylatul Qadr ni usiku wenye fadhila nyingi zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu. Usiku huu una sifa maalum na hadhi maalum sana miongoni mwa Waislamu.

Hapa kuna mambo manne kuhusu umuhimu wa Usiku wa Qadr:

Kwanza: Ukuu

"Usiku wa Qadr ni bora kuliko miezi elfu." (Aya ya 3 ya Surah Al-Qadr). Thamani maalum ya Usiku wa Qadr ni kwa sababu Qur'ani Tukufu iliteremka katika usiku huu. Iwapo watu watafahamu umuhimu wa kweli wa Usiku wa Qadr, watafaidika nao kiasi ambacho hakiwezi kuhesabiwa na mtu yeyote. Ili kufahamu ukuu wa usiku huu, inatosha kujua kwamba ni wakati ambao Qur'ani nzima iliteremshwa kwa moyo wa Mtukufu Mtume (SAW) kwa ajili ya kuwaongoza wanadamu, na kwamba ni wakati ambapo Malaika wanashuka na kuleta Baraka kwa waja weme wa Mwenyezi Mungu. Ukubwa wa Usiku wa Qadr ni kwamba Thawabu za matendo mema huzidishwa katika usiku huu.

Pili: Hesabu

Ukweli kwamba Usiku wa Qadr uko katika mwezi mtukufu wa Ramadhani ndivyo Waislamu wote wanaamini na hakuna shaka juu yake, kwa sababu Mwenyezi Mungu anasema katika Qur'ani Tukufu: "Mwezi wa Ramadhani ni mwezi ambao Qur'ani imeteremshwa." (Aya ya 185 ya Surah Al-Baqarah) na kwamba “Tuliteremsha Qur’an katika Usiku wa Qadr” (Aya ya 1 ya Sura Al-Qadr).

Mwenyezi Mungu ameificha Ijabah (kujibu maombi) katika sala zote ili watu wazisome zote kama vile alivyoficha wakati wa kifo ili kila mtu abaki tayari kwa hilo. Ndio maana tarehe kamili ya Usiku wa Qadr haijulikani. Imam Ali (AS) anasema ni kwa ajili ya waumini kuthamini nyakati za usiku na kufanya matendo mema zaidi na kuepuka madhambi zaidi na kufanya juhudi zaidi katika kumtii Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo, kuna mikesha minne ndani ya Ramadhani ambayo Waislamu wanaamini kuwa Usiku wa Qadr unaangukia moja wapo, yaani usiku wa 19, 21, 23 na 27 Ramadhani. Waislamu hukesha usiku katika tarehe hizo kuswali na kutekeleza ibada maalum.

Tatu: Kubaki Macho

Moja ya mapendekezo kuhusu Usiku wa Qadr ni kukaa macho ili kusali na kumwabudu Mungu. Kwa mujibu wa Hadithi, Waislamu wanapendekezwa kukesha hadi alfajiri, kwa sababu Usiku wa Qadr huanza kwa kuzama kwa jua na kumalizika kwa alfajiri.

Nne: Usomaji wa Qur'ani na Dua

Miongoni mwa amali zilizopendekezwa katika Usiku wa Qadr ni kusoma Qur'ani Tukufu na dua na kuomba msamaha wa Mwenyezi Mungu kwa wazazi wa mtu na waumini wengine.

Imam Baqir (AS) amesema: Kwa kila kitu kuna chemchem na chemchemi ya Qur'ani ni mwezi wa Ramadhani. Umuhimu wa Qur'ani ni mkubwa zaidi katika mwezi huu na kadhalika umuhimu wa kusoma na kutafakari Kitabu Kitukufu katika mwezi huu, hasa katika Usiku wa Qadr.

Ama kuhusu swala na dua, ifahamike kwamba katika usiku huu adhimu, waumini huwaombea wengine na kuwaombea msamaha wa Mwenyezi Mungu. Imepokewa kutoka kwa watu wakubwa wa kidini kwamba mtu anapowaombea wengine, Malaika humuombea na dua zao zina hakika kujibiwa ambapo dua zetu zinaweza zisijibiwe kutokana na dhambi zetu.

Nukta nyengine hapa ni kwamba kuna dua mbalimbali zilizosimuliwa kutoka kwa viongozi wa kidini kwa ajili ya Usiku wa Qadr ambazo zina maudhui makubwa na maana za kutia moyo. Miongoni mwao ni dua za Makarim al-Akhlaq, Jowshan, Tawbah na dua zilizotajwa katika Sahifih Sajjadiyah.

captcha