IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Qiraa ya Qur'ani ihudumie dhikri na ulinganiaji wa dini ya Mwenyezi Mungu na imani ya wasikilizaji

22:21 - April 04, 2022
Habari ID: 3475094
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema Ramadhani ni mwezi wa ugeni na rehema zisizo na kikomo za Mwenyezi Mungu, na kwamba kutakasa nafsi, kuanisika kunakoambata na kutafakari kwa kina na kuelewa vyema Qur'ani ni miongoni mwa mambo muhimu yanayomuwezesha mwanadamu kufaidika na ugeni huo wa Mola Karima.

Ayatullah Ali Khamenei ambaye Jumapili ya jana alihutubia mahafali ya qiraa ya Qur'ani katika siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, aliutaja ugeni mkubwa wa Mwenyezi Mungu katika mwezi huu kuwa unahitaji hima na juhudi kubwa ili mwanadamu aweze kujibu mwaliko wa Allah SW. Ameashiria neema na fursa za mwezi mtukufu wa Ramadhani na kusema kuwa: “Neema hizi kwa hakika ni fursa zisizo na mbadala za kuwa karibu na Mwenyezi Mungu; hivyo tunapaswa kumuomba Mwenyezi Mungu kwa unyenyekevu ili atupe taufiki ya kutumia fursa hizo na kujiepuka na madhambi.

Akinukuu Aya za Qur'ani Tukufu, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja "dhikri" kuwa ni miongoni mwa majina yaliyobarikiwa ya Kitabu kitukufu na kinyume chake ni kughafilika ambako ni balaa kubwa na akaongeza kuwa: Kusoma Qur'ani daima na kuwa karibi zaidi na kitabu hicho kunamfanya mwanadamu awe karibu zaidi na na Mwenyezi Mungu.

Ayatullah Khamenei ameitaja Qur'ani kuwa ni muujiza wa milele wa Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu, Muhammad (saw) na kuongeza kuwa: Qur'ani, katika zama zote za historia ya mwanaadamu, imemtunuku kiumbe huyo maarifa yanayohitajika katika uwanja mpana wa maisha ya mtu binafsi, familia, kijamii, kiroho kiutawala na nyanja nyigine.

Amekutaja kusoma, kutafakari kwa kina na kujifunza kuwa ndiyo siri ya kufaidika na maarifa ya kina na aali ya Qur’ani. Ameongeza kuwa: Sharti la kupata maarifa hayo ya kina ya Qur’ani ni kutakasa moyo na usafi wa roho na kwamba jambo hilo ni rahisi zaidi katika kipindi cha ujana.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza kufurahishwa na idadi kubwa ya wasomaji na maqari wazuri na hodari wa Kiirani na kusema, tunu hiyo ni matunda ya Mapinduzi ya Kiislamu. Ameongeza kuwa: "Hii leo, wasomaji Qur’ani wa Iran ni hodari na wanasoma kwa ubora wa juu zaidi kuliko wasomaji wengi kutoka nchi nyingine, ambao wakati mwingine wanaalikwa Iran kama walimu; jambo ambalo linaleta heshima na fahari."

Ameitaja qiraa ya Qur’ani kuwa ni sanaa takatifu na akasisitiza kuwa, sanaa hiyo inapaswa kuhudumia dhikri na kuwalingania watu kuelekea kwa Mwenyezi Mungu. Amesema: Kisomo cha Qur’ani  kinapaswa kufanyika kwa njia ambayo inazidishia imani ya msikilizaji; hivyo qiraa hakitakiwi kutazamwa kama sanaa tu na kuruhusu masuala yasiyo ya msingi na kujionyesha vifunike hali ya dhikri na kuwaelekeza watu kwa Mwenyezi Mungu.

4046441

captcha